Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Makubaliano hayo yenye utata baina ya nchi mbili za Rwanda na Uingereza yamelalamikiwa vikali na wabunge wa Uingereza hasa wa chama cha upinzani cha Labour ambao wamesema hautekelezeki na ni kinyume na maadili.
Makubaliano hayo yamefikiwa baina ya serikali za Kigali na London baada ya Uingereza kushindwa kufikia makubaliano kama hayo na nchi za Ghana na Albania.
Kwa mujibu wa mpango huo, kesi za wahamiaji wanaokimbilia Uingereza zitakuwa zinafuatiliwa nchini Rwanda na wakimbizi hao watashawishiwa kwenda Rwanda badala ya Uingereza.
Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson amesema kuwa, hiyo ni sehemu ya mkakati mpana wa kukabiliana na magenge ya kusafirisha watu kimagendo ambayo yanawasaidia wahamiaji na wakimbizi kujipenyeza nchini Uingereza kutokea maeneo ya bara ya Ulaya kupitia Kanali ya English.
Serikali ya Uingereza inadai kuwa Rwanda ni moja ya nchi zinazokuwa kwa kasi kubwa kiuchumi barani Afrika na inakubalika kimataifa kutokana na rekodi yake ya kupokea wakimbizi wa mataifa mbalimbali.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, serikali ya Rwanda itapewa dola milioni 158 na serikali ya Uingereza katika kile ambacho London inakiita ni ushirikiano mpana wa uhamiaji na maendeleo ya uchumi.
342/